Serikali imefungia kituo cha tiba asilia cha Foreplan kinachomilikiwa na
Tabibu Juma Mwaka Juma kwa kukiuka masharti ya kibali alichopewa kwa
kujitangaza kuwa anatoa tiba za kisasa badala ya matibabu ya asilia.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti
Wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Edmund Kayombo amesema kuwa
kituo hiko kimefutiwa usajili na hakiruhusu kutoa huduma za tiba asilia
na Tiba mbadala kwa jamii kwa kutokidhi masharti ya usajili na kufanya kazi kinyume cha usajili wake.
“Kuanzia hivi sasa tumekifutia usajili kituo cha tiba asili na tiba
mbadala cha Foreplan kwa kukiuka masharti ya usajili na hivyo
hakiruhusiwi kutoa huduma kwa jamii na watanzania kwa
ujumla”.alisisitiza Dkt. Kayombo.
Aidha Dkt. Kayombo ameongeza kuwa
vituo vingine vilivyofungiwa kutoa huduma ni pamoja na Tabibu Abdallah
Mandai wa Mandai Herval Clinic na kituo cha Fadhaget Sanitarium Clinic
kinachomilikiwa na tabibu Fadhil Kabujanja.
Dkt. Kayombo aliendelea
kwa kusema kuwa, ukiacha waliofungiwa kutoa huduma pia vipo vituo
vilivyofungiwa kwa miezi sita kila kimoja kama vile tabibu Simon Rusigwa
wa kituo cha Sigwa Herbal Clinic na Tabibu John Lupimo wa kituo cha
Lupimo Sanitarium Clinic.
Mbali na hayo Dkt. Kayombo amesema kuwa
huduma za tiba asili na tiba mbadala zinagusa zaidi maisha na afya za
wananchi moja kwa moja na hivyo sio vyema zikaachwa ziendeshwe kiholela
bila utaratibu wa kitaalamu na kimaadili.
“Kutokana na huduma hizo
kutolewa kiholela, waratibu wote mnatakiwa kufuatilia na kuchukua hatua
za kisheria dhidi ya waganga wote ambao hawajajisajili na kutoa taarifa
katika Ofisi ya Msajili wa Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kila
hatua iliyochukuliwa” aliongeza Dkt. Kayombo.
Aidha Dkt. Kayombo
amesisitiza kwamba kila mtoa huduma lazima asajiliwe yeye mwenyewe,
wasaidizi wake pamoja na kituo chake cha kutolea huduma kupitia ofisi za
Mganga Mkuu wa Halmashauri husika.
No comments:
Post a Comment