Video: Meneja Sober House aanika mazito ya Ray C
Stori: Issa Mnally na Richard Bukos
Risasi Jumamosi
Dar es Salaam: SIKU
chache baada ya kufikishwa katika kituo maaulum cha kusaidia waathirika
wa dawa za kulevya Bagamoyo Sober House, meneja wa kituo hicho, Godwin
Msilo ameeleza mazito ya mrembo huyo sambamba na maendeleo yake kwa
ujumla.
Ray C alifikishwa kwenye kituo hicho
Ijumaa iliyopita baada ya kukamatwa na polisi maeneo ya Kinondoni jijini
Dar akifanya vurugu baada ya kudaiwa kuzidiwa na ulevi wa madawa ya
kulevya.
Akizungumza na wanahabari wetu Jumanne
iliyopita katika kituo hicho, meneja huyo alisema kilichomponza Ray C
hadi arudie kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa mara ya pili baada
ya awali kupatiwa tiba katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar, ni
aina ya tiba hiyo kwani ilikuwa ikimpa mwanya wa kurudia kwenye matumizi
ya madawa hayo.
Alisema, wao wanaamini tiba sahihi ya
mtu aliyetopea kwenye madawa ya kulevya ni muathirika kufikishwa Sober
House kwani wao wanamfanya muathirika asiweze kukutana na watu wengine
wanaoweza kumshawishi arudie madawa hayo hatari.
Kwa mujibu wa meneja huyo, kitendo cha
kumpa dawa pekee (methadone) za kumtibu muathirika wa madawa ya kulevya
kisha kumuacha arejee mtaani ni tatizo kubwa lililofanyika awali kwani
kilimpa mwanya mrembo huyo kujichanganya na watumiaji wa madawa ya
kulevya mitaani.
“Huwezi kumtibu mtu kwa kumpa dawa
halafu ukamwacha muathirika arudi nyumbani, utakuwa umemjenga vipi
kisaikolojia? Kuna haja ya kumchukua muathirika kumuweka sehemu katika
kituo kama hiki, anapata dawa, akishapata dawa, anapata elimu anakutana
na madaktari wa afya ya akili, anakutana na madaktari wa saikolojia,
wanamjenga kisaikolojia.

Kuhusu maendeleo ya Ray C ambaye hadi
Jumanne iliyopita alikuwa ametimiza takriban siku tano kituoni hapo,
meneja huyo ambaye pia aliwahi kuwa muathirika wa madawa ya kulevya
kabla ya kutibiwa, alisema mrembo huyo kwa sasa anaendelea vizuri.
“Yeah! Ameanza vizuri tiba, anaendelea
vizuri kwa kweli. Naamini kadiri anavyoendelea atakuwa vizuri zaidi.
Kuna mabadiliko makubwa ameanza kuyaonesha,” alisema Msilo huku akidai
muda wa kuwepo kwenye nyumba hiyo utategemeana na jinsi Ray C
atakavyoonesha kupona.
Akijizungumzia yeye kama mfano wa
watumiaji waliotopea na kisha kutibiwa, Msilo alisema licha ya kuwa yeye
alikuwa mwanajeshi kwa muda mrefu, alijikuta ametopea kwenye madawa
hayo lakini tiba pekee iliyomfanya ajinasue kwenye madawa hayo ni Sober
House.
“Mimi nilikuwa mwanajeshi kwa takriban
kama miaka 10 na kitu lakini nilifukuzwa jeshi kutokana na matumizi ya
madawa ya kulevya, nikaenda kutibiwa Kigamboni, kwa sasa nipo freshi
kabisa.
“Naomba Mwenyezi Mungu anisimamie
nisiweze kurudia maana yeye ndiye anayetusaidia kuweza kufikia malengo
yetu, sisi tunapanga lakini yeye ndiye anayetuwezesha,” alisema Msilo.
Kabla ya kufikishwa kituoni hapo, Ray C
alipoanza kuripotiwa na magazeti ya Global Publishers kwa mara ya kwanza
kuhusu kutopea kwenye madawa ya kulevya, wadau mbalimbali waliguswa na
hali mbaya aliyokuwa nayo kitendo ambacho kilimgusa rais mstaafu, Jakaya
Kikwete aliyemuita ikulu na kumsaidia.
No comments:
Post a Comment